Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga inatekeleza programu mbalimbali zinazolenga kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, hifadhi ya mazingira, udhibiti wa taka na utunzaji wa vyanzo vya maji kama kaulimbiu ya Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2024 inavyosema.

Afisa Mazingira wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi Bw. Rodgers Shemahonge akizungumzia wakati wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2024 amesema halmashauri inatekeleza kigezo namba 10 kinachohusu Hifadhi ya Mazingira na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Amesema kwa kipindi cha miaka mitano halmashauri imepanda miti milioni 7.5 na miti iliyopona ikiwa zaidi ya milioni tano sawa na asilimia 76.3 ya miti iliyopandwa.

“Pia halmashauri ina vyanzo vya maji 28, visima virefu 8, mabwawa Matano, maji mtiririko 5 na visima vifupi 10 huku miti 8,193 ikipandwa katika vyanzo vya maji na iliyopona ni miti 6,461.

“Halmashauri ya Kilindi ina jumla ya hifadhi za milima 63 zenye hekta 40,474 ambapo zinapatikana katika misitu ya hifadhi. Aidha Kilindi ina jumla ya mito 17 huku minne ikiwa inatiririsha maji mwaka mzima na mito 13 ni ya msimu,” amesema Bw. Shemahonge.

Ameongeza kuwa Kilindi inasimamia na kudhibiti taka ngumu katika vijiji, mitaro, masoko, vituo vya mabasi, madaraja na mazingira ya jamii.

Kwa upande wake Afisa Msitu Ofisi ya Makamu wa Rais Bw. Timotheo Mande ameongeza kuwa halmashauri hiyo pia imejitahidi katika kujiwekea mikakati ya kuhakikisha inadhibiti ufugaji katika maeneo yasiyo rasmi na kuzuia uchimbaji madini usiokuwa endelevu.

By admin

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *