Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe Dkt. Selemani Jafo akifanyiwa mahojiano na Shirika la Utangazaji la Zanzibar (ZBC), Aprili 2,2024 ambapo amezungumzia umuhimu wa utunzaji wa mazingira ikiwa pamoja na jitihada zinazochukuliwa na serikali za kukabiliana na uharibifu wa mazingira.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Waandishi wa Habari katika Uwanja wa Ushirika Moshi baada ya mahojiano wakati wa uzinduzi wa Mbio za Mwenge kitaifa, Aprili 2,2024.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa akiwasha Mwenge wa Uhuru katika Uwanja wa Ushiriki mkoani Kilimanjaro, Aprili 2,2024 ambapo amesisitiza wananchi juu ya utunzaji wa Mazingira na kuepuka uchomaji Misitu na uharibifu wa vyanzo vya maji.

=========================================================================

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo ameendelea kuhimiza matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kukabiliana na uharibifu wa mazingira kutokana na ukataji wa miti.

Ametoa rai hiyo alipokuwa akizungumza na vyombo mbalimbali vya habari wakati wa uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2024 katika Uwanja wa Chuo cha Ushirika Moshi mkoani Kilimanjaro uliofanywa na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa leo Aprili 02, 2024.

Dkt. Jafo amesema kuwa Serikali ilitangaza kusitisha matumizi ya kuni na mkaa kwa taasisi zinazolisha watu zaidi ya 100 kuanzia Januari 2024 ambapo tayari taasisi hizo zimetekeleza maelekezo hayo.

Amesema kuwa kila mwaka takriban hekta laki nne za misitu zinapotea kutokana na kukatwa kwa ajili ya kuni na mkaa hivyo Serikali inahamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kuinusuru.

“Utunzaji wa mazingira unagusa mambo mengi, hivi karibuni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan alizindua Kampeni ya Nishati Safi ya Kupikia ili kuhifadhi mazingira,“ amesisitiza.

Aidha, Waziri Jafo amesema kuwa Mwenge wa Uhuru mwaka huu umeleta faraja kubwa katika utunzaji wa mazingira kwani utakimbizwa mikoa yote hivyo utasaidia wananchi kuelewa dhana nzima ya utunzaji wa mazingira na changamoto kubwa kwa sasa ni utunzaji wa mazingira

Itakumbukwa kuwa katika kilele cha Mwenge wa Uhuru 2023 kilichofanyika Oktoba 14 mkoani Manyara, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango alitoa rai kwa Ofisi ya Waziri Mkuu kuendelea kutumia ujumbe unaohamasisha jamii utunzaji wa mazingira ili kusaidia kulinda na kutunza Mazingira.

Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2024 una kaulimbiu “Tunza Mazingira na Shiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa Ujenzi wa Taifa Endelezu” ambayo inaweka msisitizo kwa namna nyingine katika uhifadhi wa mazingira. 

By admin

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *